MATUKIO MUHIMU YA MWAKA

NA SONGEA INAPANIA KUWA MMISIONARI: Tarehe 18 Aprili Songea ilishuhudia umati wa waumini waliomiminika na kufurika katika uwanja wa Zimanimoto mjini Songea ili kushiriki katika Kongamano la Uenjilishaji au Umisionari. Waumini wengi waliotoka hasa Maparokia ya mjini Songea, yaani: Parokia ya Mt. Theresia wa Mtoto Yesu Matogoro, Parokia ya Mt. Mathias Kalemba Mulumba ya Songea, Parokia ya Familia Takatifu ya Bombambili, na Parokia ya B. Maria Aliyepalizwa Mbinguni ya Mji Mwema. Pia walijiunga waumini wachache wa maparokia mengine na watu wengine wa madhehebu mengine ya dini. Wamisionari wetu wakongwe na maarufu wa Peramiho, wa Hanga, wa Chipole, na Waaugustiniani wa Mahanje na Wino na watawa wa mashirika mbalimbali walihudhuria kwa wingi sana. Kongamano lilitokana na mpango wa Baraza la Maaskofu wa kutualika Majimbo mbalimbali kushiriki katika Kongamano hilo ili kuhamasisha roho ya utangazaji Enjili au roho ya umisionari kwa daima, na pia ilikuwa ni nafasi ya kutafakari kwa kina juu ya kazi nzuri na kubwa ya umisionari iliyokwisha kutendeka katika eneo hili letu, yaani katika Jimbo Kuu la Songea. Maandalizi na adhimisho la Kongamano hili lilihamasishwa hasa na Kamati ya Uenjilishaji (MAC) ya Baraza la Maaskofu iliyokuwa imeanzishwa na Umoja wa Mashirika ya watawa wanaume. Katika Misa Takatifu iliyoadhimishwa siku hiyo uwanjani Zimani moto, tayari Makatekista 14 walijitokeza na kujieleza kwa Askofu hiari yao ya kwenda missioni na kufanya kazi huko kwaajili ya watu. Na vijana wengine wanne waliamua kujitolea kuwatunza na kuwasaidia mapadre wa Jimbo wanapougua na kulazwa hospitalini. Roho wa Bwana yu juu yetu ili tuwahubirie watu Enjili ya Kristu.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

MAADHIMISHO YA KIPAIMARA:

Mapema mwezi Mei Watoto wa Darasa la sista wa St Agnes Chipole Walipata Sakramenti ya Kipaimara katika Kanisa la Chipole.

Tarehe 19 Juni 2004 iliadhimishwa Sakramenti ya Kipaimara katika Kanisa la Parangu kwa Wanaparangu na tarehe 20 Juni iliadhimishwa katika Kanisa la Peramiho kwa watoto wa Peramiho A na Likuyu Fussi.

 

 

CHIPOLE UTAWANI: Tarehe 24 Juni 2004 Wana- Agnes, wakijumuika na waumini waliofurika toka sehemu mbalimbali wamekuwa na sherehe kubwa ya Jubilei ya miaka 25 ya nadhiri kwa Masista kumi na moja. Masista Wanajubilei ni:

1. Sr. Mfurahivu Kinyero OSB, 2. Sr. Hisani Mhagama OSB, 3. Sr. Sistahili Sowo OSB, 4. Sr. Agnesia Ndunguru OSB, 5. Sr. Ines Hyera OSB, 6. Sr. Lwanga Nchimbi OSB, 7. Sr. Mwangavu Mbunda OSB, 8.Sr. Achilles Sanga OSB, 9. Sr. Blanca Gowele OSB, 10. Sr. Safina Komba OSB, na 11. Sr. Chrisma Ngonyani OSB. Tunawatakia Heri sana, Tunawabariki na tunawaombea.